Hatia

Ah! Sikuwa na zali sikuziamini ndumba
Sikuwa na mali za kufuja
Nilijitahidi kuuza mitumba kufuga mipunga
Ili siku nimpe gari nimpe nyumba. Nilishindwa...

Niliishia kumpa chai, 'chipsi' mayai na 'vocha'
Nywele za kimasai na mkoba
Pesa za magauni, majuba na viatu vya kuzuga
Nilimpa muda ila bado haikutosha, kwani...

Nilipomwambia nampenda hakujibu
Akaweka moyo wangu maumivu
Na mtima wangu akauweka 'solemba'
Nikaapia kuwa sitakuja kupenda 'forever'

Ah! Nilimpa upendo nilimpa sifa
Niliweka mitego ya faida, haikuwa shwari
Nikabadili mwenendo wa maisha
Niliweka malengo sikutimiza, hakunikubali

Alikuwa na ndoto kubwa kushinda mimi
Alikuwa na misimamo kuipita dini
Aliniambia ameomba nije kuokota utajiri
Amengoja sana na sasa amechoka kusubiri

Ah! Sikuwa na hali ya kuikosha roho yake
Nilimwacha aende aufate moyo wake
Alipata bwana wa kizungu magharibi
Alimwahidi kuishi maisha ya ndoto zake

Nilipata uchungu niliishia kuhamaki nilitaka nijiue
Nilitaka nimzuie abaki nikakumbuka
Ukipenda ua haulikati unaliacha likue

Duka langu nilifunga biashara niliacha zote
Uchumi uliyumba kwa maana nilianza pombe
Niliumwa bado kidogo moyo uzime
Nilimfanya ndoto kumbe naye ana ndoto nyingine

Alisema anakwenda jiji la Miami
Hakuna alichowaza zaidi ya kuishi kifahari
Kamtumia picha na 'mchizi' kazikubali
Na yupo tayari kumlipia gharama za safari

Aliondoka na kipande kimoja cha mwili
Nilikonda nilipata ugonjwa wa akili
Haikuwahi kupita hata sekunde nisilie
Nilitamani mpaka ardhi ipasuke niingie

Ah! Muda ukaenda nitapata 'Mwanamwali'
Nikamwomba awe mwenza wa maisha akakubali
Nikamvisha pete nikalipia mahari
Sikumpenda lakini nilijifunza kumjali

Aliuliza kama nampenda, nilimjibu
Sikutaka kuweka moyo wake maumivu
Sikutaka kuuweka Mtima wake solemba
Kiasi aseme hatakuja kupenda "forever"

Ah alinikumbatia nikamfunga kwa ishara
Akanikabidhi tunda nikala
Akaniamini tukajuana nikapanga kumwoa
Akaidhisha na tukaanza na mipango ya ndoa

"Habari naamini u bukheri wa afya
Unaendeleaje maisha na huyo mpenzi wa sasa
.Nashukuru nahema ughaibuni si kwema
Nakiona cha mtema mpaka naona ni heri nikafa...

Ah! Maisha niliyowaza yote ni uongo
Nauzishwa madawa nalazimishwa ngono
Nafungiwa ndani kama mtumwa ufungwani
Roho yangu rehani kiasi sasa naitamani Bongo

Ukubwa umekuja kunisafisha jicho
Ndoto imeisha na taswira imenionyesha sivyo, ah
Naomba unifate uniondoshe kwenye hichi kifo
Na hii namba ya msamaria atakueleza nilipo"

Sherehe ilikuwa na mipango madhubuti
Kabla mimi kuichukua michango ya Harusi
Nikatoroka ughaibuni kufuata hisia zangu
Kwenda kumfata njiwa wangu mahususi

Nilivuka majangwa na majabali
Sehemu ya safari anga sehemu nyingine bahari
Niliacha kila kitu nyuma upendo na huruma vilinijaa
Penzi likanipeleka mbali

Nikakutana na bopa la kizungu
Lenye sura ya kuichachisha mboga kwenye chungu
Kiko kwenye mdomo,Tatuu kila kona na wapambe
Pamoja na vishoka wenye mtutu

Sio siri alizungukwa na wasichana wengi
Sikujua umri walikuwa wadogo ka' "madent"
Baadhi walikuwa uchi wanahesabia "chenchi"
Wengine masaji huku wengine wanamchezea nyeti

Hata nilipomuuliza kama ananipenda hakujibu
Akaweka moyo wangu maumivu
Nilijua hawezi kufa kwa sababu hakunipenda
Na ni rasmi nikapoteza shilingi kwenye msitu

Nilikiambia kifo kama unakuja njoo
Maana sikuwa mtu ilishakufa roho
Sikuumia kama alivyoniumiza yeye
Kwahiyo sikujali jinsi nilivyoteswa na wale mbwa no

Aliambiwa ambusu bosi hakubisha
Alipewa bunduki hakusita
Aliishika risasi akaiingiza
Akaambiwa anipige kwenye kichwa



Credits
Writer(s): Edger Mwaipeta
Lyrics powered by www.musixmatch.com

Link